Kahama FM
Kahama FM
27 October 2026, 4:32 pm

‘‘Halmashauri nyingine zilizopo wilayani Kahama zatakiwa kuendelea kutoa mikopo ya 10% kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu’’
Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama mkoani Shinyanga imekabidhi mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 526.6 kwa vikundi 36 vya wajasiriamali kupitia fedha zinazotengwa kwa utaratibu wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Makabidhiano hayo yameongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Dkt. Francis Mlacha, katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Msalala, Kata ya Ntobo, ambapo amewataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kukuza mitaji yao, kuinua uchumi na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Aidha, Dkt. Mlacha amezitaka halmashauri nyingine zilizopo wilayani Kahama kuendelea kutoa mikopo hiyo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, akisisitiza umuhimu wa kutekeleza agizo la Serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya makundi hayo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila, amesema mikopo hiyo itasaidia kuongeza mnyororo wa thamani, hususan katika sekta ya kilimo, pamoja na kuchochea uanzishwaji wa viwanda vidogo vitakavyoongeza uzalishaji wenye tija na kukuza uchumi wa wananchi.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Husna Toni, amesema halmashauri hiyo itaendelea kutekeleza mpango huo, huku akibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 wanatarajia kutenga Shilingi milioni 800 kwa ajili ya mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameipongeza Serikali kwa kuwawezesha kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi, huku wakiahidi kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati ili wananchi wengine waweze kunufaika.
