Kahama FM
Kahama FM
22 October 2026, 8:32 am

‘‘Wananchi mwendakulima wataka eneo la makaburi ya umma kuainishwa kwenye Mpango Kabambe’’
Wananchi wa Kata ya Mwendakulima katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, wameiomba Serikali kuhakikisha eneo lililotengwa kwa ajili ya makaburi ya umma linaainishwa wazi katika Mpango Kabambe wa mji ili kuzuia migogoro ya ardhi na udanganyifu katika uuzaji wa viwanja.
Wakizungumza katika kikao cha Kupanga Kahama ya Baadaye, wananchi hao, akiwemo Shabani Mapinda, Selemani Kishimba na Besa Emmanuel, wamesema ni muhimu eneo hilo kuonekana wazi katika ramani ya matumizi ya ardhi ili kuwawezesha wananchi kutambua maeneo yaliyotengwa kwa matumizi maalumu na kuepuka kununua viwanja visivyoruhusiwa kwa makazi.

Wamesisitiza kuwa utambuzi wa mapema wa eneo hilo utasaidia kulinda maeneo ya makaburi ya umma na kuzuia changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa Mpango Kabambe.
Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa Maendeleo ya Jamii na Usalama kutoka kampuni ya Urban Solution, Novatus Kaijage, amesema kupitia Mpango Kabambe, wataalamu wa mipango miji wanapaswa kuhakikisha taarifa za matumizi ya ardhi zinawekwa wazi na kupatikana kwa wananchi ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi kabla ya kununua viwanja.

Katika hatua nyingine, Kaijage amesisitiza umuhimu wa upangaji mzuri wa maeneo ya miji, akieleza kuwa matumizi ya ardhi yanapokosa utaratibu maalumu, hali hiyo inaweza kusababisha migongano kati ya wananchi wanaohitaji ardhi kwa ajili ya makazi, kilimo, ufugaji, viwanda na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo, utekelezaji wa maombi hayo unahitaji tathmini na hatua za mamlaka husika katika kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa matumizi mbalimbali yanatambuliwa na kuainishwa ipasavyo, huku wananchi wakiendelea kushiriki katika kutoa maoni kuhusu Mpango Kabambe unaolenga kuujenga mji wa Kahama uliopangwa vizuri na kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi.
