Kahama FM
Kahama FM
4 November 2026, 2:36 pm

Kata ya Malunga yaungana na Manispaa ya Kahama katika kupanga mustakabali wa Kahama kuwa mji wa kisasa kwa mifumo ya kidijitali
Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imeendelea kutoa elimu na kushirikisha wananchi katika maandalizi ya Mpango Kabambe wa Kahama ya Kidijitali, unaolenga kuboresha matumizi ya ardhi na kuweka misingi ya maendeleo ya mji kwa kuzingatia mifumo ya kisasa.
Kupitia mkutano uliofanyika katika Kata ya Malunga, wananchi na viongozi wa maeneo hayo wamepata fursa ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mipango ya matumizi ya ardhi na maendeleo ya mji.

Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Habari na Mawasiliano wa Mradi wa Mpango Kabambe wa Kidijitali, Hamisi Mkoma, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika kuboresha mipango ya maendeleo ya Kahama, akieleza kuwa ushirikishwaji wa wananchi ni msingi muhimu wa kuhakikisha mpango huo unakidhi mahitaji ya jamii.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Malunga, Yasinta Kimaro, amesema uelewa na ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo na kuhakikisha matumizi bora ya ardhi kwa manufaa ya jamii.

Naye Afisa Elimu wa Kata ya Malunga, Matrida Masuke, amesema kumekuwa na ushirikiano kati ya Manispaa ya Kahama na wananchi katika kufanikisha mpango huo, huku akiwataka wananchi kuzingatia mipango iliyowekwa katika utekelezaji wa shughuli zao za maendeleo.
Mpango Kabambe wa Kahama ya Kidijitali ni sehemu ya jitihada za Manispaa ya Kahama za kuelekeza ukuaji wa mji katika misingi ya kisasa, ikiwemo matumizi bora ya ardhi na teknolojia katika usimamizi wa taarifa za mipango miji.
