Kahama FM
Kahama FM
5 October 2026, 12:15 pm

”Wananchi chukueni hatua za mvua za EL NINO kwa kufanya usafi katika mitalo yenu iliyo kwenye nyumba zenu”
Wananchi mkoani Shinyanga wametakiwa kuchukua tahadhari kwa kuweka mazingira salama na kuhama katika maeneo ya mikondo ya maji, kutokana na uwezekano wa kunyesha kwa mvua kubwa, huku Serikali ikiendelea kuhakikisha miundombinu iko katika hali nzuri na salama.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, wakati wa ziara yake wilayani Kahama kwa ajili ya kukagua miundombinu pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi, ambapo amesema kila mwananchi anapaswa kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.

Aidha, amesisitiza wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, hususan kandokando ya mikondo ya maji, kuchukua hatua mapema kwa kuhama ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.
Kwa upande wake, meneja wa TARURA wilaya ya Kahama Mhandisi Joseph Mkwizu amesema kuwa wameboresha matalo mkubwa wa maji unaokusanya maji mengi katika mjini wa Kahama, ambapo kukamilika kwake utasaidia kupunguza athari za mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni.

Awali, baadhi ya wananchi wa kata ya Mhongoro akiwemo Alex Adof na Regunda Paulo wamesema wamejiandaa kwa mvua za El Nino kwa kuchimba mitalo na kuweka mifuko ili kuzuia athari za mvua hizo, huku wakiiomba serikali kuendelea kutengeneza miundombinu ya barabara na mitalo pamoja na kuelekeza maji kwenye maeneo ambayo sio makazi ya watu.
Diwani wa kata ya Mhongolo Mariam Galula ameishukuru serikali kwa kuongeza kuujenga urefu wa mtalo hio, ambapo umekuwa kuleta athari kwa wananchi zinaponyesha mvua kubwa hali inayosababisha baadhi ya nyumba kuingiliwa maji.
