Kahama FM

Serikali imefuta kodi ya uagizaji saruji na malighafi zake

9 November 2026, 12:32 pm

Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kishapu katika mkutano wa hadhara (Picha na Sebastian Mnakaya)

”atua hiyo inatarajiwa kusaidia bei ya saruji kushuka na kurejea katika hali ya kawaida”

Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali imefuta kodi ya uagizaji wa saruji kutoka nje ya nchi pamoja na malighafi zinazotumika kuizalisha, hatua inayolenga kupunguza gharama za ujenzi na kushusha bei ya bidhaa hiyo.

Ametoa kauli hiyo Novemba 8, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kishapu katika mkutano wa hadhara, akieleza kuwa Serikali inatambua changamoto ya kupanda kwa bei za vifaa vya ujenzi.

Amesema hatua hiyo inatarajiwa kusaidia bei ya saruji kushuka na kurejea katika hali ya kawaida, huku Serikali ikiendelea kushughulikia gharama za bidhaa na huduma muhimu.

Sauti ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Paschal Katambi, kuhakikisha wananchi wanaofanya makosa ambayo adhabu yake ni faini wanatozwa faini bila kushikiliwa vitendea kazi vyao.

Dkt. Mwigulu amesema kushikiliwa kwa bodaboda, bajaji na magari ya wananchi kwa muda mrefu kunawanyima fursa ya kuendelea kuzalisha kipato, hali inayoweza kuwafanya washindwe kulipa faini wanazodaiwa.

Sauti ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba

Amesisitiza kuwa mamlaka zinapaswa kuheshimu mitaji ya wananchi kwa kuwa baadhi ya vitendea kazi hivyo vimenunuliwa kwa mikopo na ni tegemeo la kujipatia kipato na kuendesha familia zao.