Kahama FM
Kahama FM
26 November 2026, 5:50 pm

‘‘Maandalizi haya yanatarajia kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa miundombinu ya elimu na kuhakikisha wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028 wanapata nafasi za masomo katika mazingira bora’’
Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga inatarajia kupokea wanafunzi zaidi ya 25,113 wanaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028, hatua inayohitaji maandalizi ya mapema ya miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa ili kukabiliana na upungufu wa vyumba 246.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani, Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kahama, Anastazia Manumba, amesema ongezeko hilo la wanafunzi linatokana na mabadiliko ya mfumo wa elimu ambapo mwaka 2027 kutakuwa na makundi mawili ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi, wakiwemo wanafunzi wa darasa la sita na la saba.

Amesema hali hiyo inahitaji ushirikiano wa viongozi na wadau wa elimu katika kuanza ujenzi wa madarasa na kuanzisha shule mpya za sekondari ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapata nafasi za kuendelea na elimu.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Abuslamu, amewataka viongozi na wadau mbalimbali kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao, hususan kuboresha miundombinu ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.

Naye Diwani wa Kata ya Nyahanga, Josephina Kilimba, amesema kata hiyo imeanza maandalizi ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari, ambapo katika awamu ya kwanza wanatarajia kujenga vyumba 14 vya madarasa na kuongeza vyumba vingine 14 katika awamu inayofuata, huku wakilenga kukamilisha ujenzi huo ifikapo Juni 2027.

Akizungumzia utekelezaji wa mikakati hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masud Kibetu, ameeleza hatua zinazochukuliwa na kata mbalimbali katika kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa lengo la kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Maandalizi hayo yanatarajiwa kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa miundombinu ya elimu na kuhakikisha wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028 wanapata nafasi za masomo katika mazingira bora.