Kahama FM

Manispaa ya Kahama yatoa bilioni 2.16 za mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi 96

5 November 2026, 11:23 pm

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita akikabidhi mfano wa hundi wa shilingi bilioni 2.16 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa mikopo ya asilimia 10 (Picha na Sebastian Mnakaya)

Halmashauri ya Kahama yatoa bilioni 2.16 za mikopo kwa vikundi 96 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu

Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imetoa zaidi ya shilingi bilioni 2.16 kwa vikundi 96 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Akikabidhi mfano wa hundi ya fedha hizo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amewataka vijana na makundi mengine yanayonufaika na mikopo hiyo kutumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi, akieleza kuwa mikopo hiyo haina riba na ina masharti rafiki.

Sauti ya , Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita

Aidha, Mhita amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa Manispaa ya Kahama kuendelea kutoa elimu kuhusu mikopo hiyo na kuhakikisha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yanapata fursa ya kunufaika nayo ili kupunguza utegemezi wa mikopo yenye masharti magumu na riba kubwa.

Sauti ya , Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masod Kibetu akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Kahama

Akisoma taarifa ya utoaji wa mikopo hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masod Kibetu, amesema jumla ya vikundi 96 vimepatiwa mikopo hiyo, ambapo vikundi 45 ni vya vijana, vikundi vitano vya watu wenye ulemavu na vikundi 46 vya wanawake.

Sauti ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masod Kibetu

Kwa upande wao, baadhi ya vijana walionufaika na mikopo hiyo katika Manispaa ya Kahama, akiwemo Jonathan Joel, Abdala Ramadhan Salum na Paul Damasi, wamesema mikopo hiyo imekuwa mkombozi kwao ikilinganishwa na mikopo ya taasisi nyingine za kifedha ambayo awali walikuwa wakiipata kwa riba kubwa.

Wamesema kupitia mikopo hiyo isiyo na riba, wamepunguza gharama za marejesho na kupata fursa ya kuelekeza fedha nyingi zaidi katika kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Sauti za wanufaika ya mikopo ya asilimia 10 Jonathan Joel, Abdala Ramadhan Salum na Paul Damasi