Kahama FM
Kahama FM
20 July 2026, 11:37 pm

‘‘Dereva atakaye jaza mafuta na abiria wakiwa ndani ya gari atapatiwa adhabu’’
Baadhi ya madereva wa magari ya abiria wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuzingatia kanuni za usalama katika vituo vya mafuta kwa kuhahikisha hawajazi mafuta wakiwa na abiria ndani ya gari.
Wito huo umetolewa na Kaimu mkuu wa usalama barabarani wilaya ya Kahama, mrakibu msaidizi wa jeshi la polisi (ASP) Amani Katumbo, wakati akizungumza na Kahama Fm, ambapo amesema kuwa ni kosa kisheria kwa dereva yoyote kujaza mafuta na abiria wakiwa ndani ya gari, na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, afande Amani amesema kuwa jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani wameendelea kutoa elimu, huku wakiwataka wananchi kuripoti matukio ya namna hiyo ili kupunguza na kuondokana na ajili zisizokuwa za lazima.
Kwa upande wake mwenyekiti msaidizi wa stendi kuu ya mabasi Kahama, John Riziki ameeleza changamoto wanazokutana nazo madereva ikiwa kukosa mitaji hali inayosababisha baadhi yao kujaza mafuta baada ya kupata abiria, huku akiomba elimu iendelee kutolewa zaidi.

Nao baadhi ya abiria katika Manispaa ya Kahama, akiwemo Isack Donard na Maria Joel wamesema baadhi ya abiria wamekuwa wakikaidi agizo la kushuka kwenye gari inapotea dharura ya kujaza mafuta, huku wakiomba madereva na abiria kufuata sheria ili kuondokana na changamoto itakayojitokeza.
Hata hivyo, katika sheria za usalama barabarani haziruhusu gari ya abiria kujaza mafuta ikiwa imebeba abiria, na dereva atayebainia kufanya hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.