Chai FM

Sheria yalenga kuhifadhi na si kunyang’anya ardhi ya wananchi Busokelo

17 April 2025, 10:22 am

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kanyelele wakifuatilia kwa makini elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji (picha na Sabina Martin)

Uwepo wa sheria ya uhifadhi wa mazingira namba 20 ya mwaka 2004 inalenga kuhifadhi mazingira na si vinginevyo.

Na Sabina Martin- Rungwe

Imeelezwa kuwa uwepo wa sheria ya mazingira inayokataza shughuli za kibinadamu ndani ya mita sitini kutoka katika chanzo cha maji  ni kutunza na kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na vyanzo vya maji na si kunyang’anya ardhi ya wananchi.

Hayo yameelezwa na Bw. Paul Maganga afisa ardhi halmashauri ya wilaya ya Busokelo wilayani Rungwe mkoani Mbeya katika mkutano na wananchi wa kijiji cha Kanyelele kata ya Kabula wenye lengo la kuwashirikisha wananchi juu ya uwekaji wa alama za mipaka katika vyanzo vya maji zoezi linalofanywa na bodi ya maji bonde la ziwa nyasa.

Sauti ya Afisa ardhi Busokelo

Afisa kilimo halmashauri ya Busokelo Bw. Fadhili Mgaya akatumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa wananchi wa kijiji cha kanyelele kutopeleka mifugo yao katika maeneo yote yaliyo hifadhiwa, maeneo ya taasisi pamoja na maeneo ya vyanzo vya maji.

Sauti ya afisa kilimo Busokelo

Kwa upande wake Masanja Jihangala ambaye ni afisa mazingira halmashauri ya Busokelo Amesema kwamba kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 imeainisha faini ya shilingi elfu hamsini hadi milioni hamsini kwa mtu yeyote atakaye haribu mazingira ikiwa ni pamoja na vyanzo vya maji.

sauti ya afisa mazingira Busokelo

Akizungumzia madhara ya upandaji wa miti isiyorafiki katika vyanzo vya maji mhifadhi misitu halmashauri ya Busokelo Bw.Ndyamasa Rubuye amesema miti aina ya mkaratusi hunywa maji lita 7,300(elfu saba na miatatu) mti mmoja kwa mwaka sawa na lita ishirini kwa siku, wakati mti aina ya mkambo kambo ukinywa maji lita 5,600(elfu tano na miasita) kwa mwaka sawa na lita 15 kwa siku kwa mti mmoja.

Sauti ya Mhifadhi misitu Busokelo

Bi. Chiwaya Nkomola ni afisa maendeleo ya jamii kutoka bodi ya maji bonde la ziwa nyasa katika mkutano huo amesema kwamba bonde la ziwa nyasa pamoja na mambo mengine wapo kwaajili ya kutunza, kulinda, kuhifadi na kuviendeleza vyanzo vya maji kwa matumizi ya vizazi vya sasa na vijavyo huku akisisitiza kuwa kwa sasa hatua itakayofuata baada ya kutoa elimu kwa jamii ni kuweka mipaka katika chanzo cha maji cha mto nyelele.

Sauti ya afisa maendeleo bodi ya maji bonde la ziwa Nyasa

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji hicho mara baada ya kupatiwa elimu na kushirikishwa juu ya zoezi la uwekaji wa mipaka katika chanzo cha maji cha mto nyelele wameomba busara itumike huku wakiomba muda wa mwaka mmoja ili kila mwananchi akate miti isiyorafiki katika chanzo hicho.

Sauti za wananchi wa Kanyelele Busokelo

Ikumbukwe kwamba Sekta ya maji ni sekta mtambuka hivyo ili kuhifadhi rasilimali maji inahitaji ushirikiano wa pamoja na wataalam mbalimbali wa sheria, misitu, maji, mazingira, ardhi, kilimo pamoja na wananchi wenyewe kwani maji yaweza kuwepo bila binadamu wakati bindamu hawezi ishi bila maji.