Chai FM

Mbolea ya ruzuku kilio kwa baadhi ya wakulima

16 December 2022, 12:16 pm

RUNGWE- MBEYA NA JUDITH MWAKIBIBI

Kutokana na kukosekana kwa mbolea ya ruzuku kwa baadhi ya maeneo Wilaya Rungwe Mkoani Mbeya wakulima wametakiwa kuwa na subira wakati serikali ikiendelea kulishughulikia suala hilo.

Hayo yamebainishwa na afisa kilimo wilayani hapa Bw Juma Mzara wakati akizungumza na kituo hiki amesema kuwa changamoto hiyo imewafikia wao kama idara ya kilimo na wamefuatilia  hadi kwa mawakala na kugundua kuwa kuna changamoto ya makampuni kuto peleka mbolea ya kutosha kwa mawakala.

Aidha Mzara idara imeagiza mawakala kuwasisitiza makampuni kuendelea kuongeza kasi ya uagizaji wa mbolea ya ruzuku kwani mbolea iliyopo sasa sio toshelezi kwa wakulima wa Rungwe kutokana na baadhi ya wilaya kuchukua mbolea wilayani hapa.

Hata hivyo amesema hadi mwezi Novemba mwaka huu wakulima waliopata mbolea ni elfu 32 na bado walikuwa wanaendelea kusajili katika mfumo hivyo kufanya idadi ya wakulima waliopata mbolea ya ruzuku kuongezeka.

Katika hatua nyingine ametoa wito kwa wakulima kuwahi pindi wanapo pata taarifa ya kufika kwa mbolea ya ruzuku kwa mawakala wenye vibali vya kutoa mbolea.