Chai FM

CHADEMA: Wananchi washughulikie viongozi wazembe

11 September 2023, 12:00 pm

katibu wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kanda ya nyasa Gwamaka Mbugi akihutubia wananchi hawapo pichani( picha na mwandishi wetu)

Kuelekea uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa 2024 vyama vya upinzani wameeleza mbinu watakazozitumia kuking’oa chama tawala madarakani.

Na Cleef Mlelwa- Makambako

Wananchi wa halmashauri ya mji wa Makambako wametakiwa kuwaondoa madarakani viongozi wote wa kisiasa ambao wameshindwa kutatua changamoto zao na kusimamia fedha za serikali katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais 2025.

Wito huo umetolewa na katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa Gwamaka Mbugi katika mkutano wa hadhara na wananchi wa mtaa wa Mangula kata ya Mjimwema mjini Makambako wilayani Njombe, ambapo amesema wananchi wana haki ya kuwaondoa viongozi wote ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao kwa kupiga kura.

Gwamaka amesema changamoto za ubadhirifu wa fedha za serikali kwenye halmashauri nyingi nchini unasababishwa na madiwani pamoja na wabunge ambao wameshindwa kuwasimamia wataalam kwenye halmashauri zao.

Sauti Gwamaka Mbugi katibu CHADEMA Kanda ya Nyasa

Wakizungumza katika mkutano huo mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Njombe Rose Mayemba na Katibu wa chama hicho Baraka kivambe wamesema iko haja ya kubadilishwa kwa mifumo ya uendeshaji wa nchi ikiwemo katiba ili sekta ya kilimo ilete tija kwa jamii.

Nao baadhi ya wanachama wa chama hicho jimbo la Makambako wamesema ili kuboreshwa kwa huduma mbalimbali za kijamii hasa kwa sekta za kilimo, afya na maji ni lazima kuwepo viongozi wenye uwezo wa kuwasemea wananchi changamoto zao na kuzitatua.