Chai FM

Jamii kukabiliana na ukatili mtandaoni Rungwe

9 May 2024, 1:16 pm

Kutokana na kuwepo kwa vitendo vya ukatili mtandaoni dhidi ya watoto wazazi na walezi watakiwa kuwa mstari wa mbele katika malezi kwa watoto

Na Noah Kibona

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imeendesha kampeni maalumu dhidi ya Usalama wa Watoto Mitandaoni lengo mahususi likiwa ni kuwajengea ustawi bora watoto na kuwaepusha vihatarishi vinavyoweza kurudisha nyuma makuzi stahiki na malezi katika jamii.

Kampeni hiyo imefanyika katika shule ya Msingi Tukuyu lengo likiwa ni kuzifikia shule 9 zaidi ndani ya halmashauri.

Afisa maendeleo ya jamii kutoka wizara ya jamii,jinsia,wanawake na makundi maalum Christabela Ngowi akitoa elimu juu ya ukatili kwa watoto mtandaoni

Christabela Ngowi ni Afisa Maendeleo Mkuu kutoka katika Wizara hii ambapo ameikumbusha jamii kuhakikisha inawakinga Watoto na Mitandao ya kijamii hasa picha au vielelezo vinavyokinzana na Mila na desturi zetu pamoja na sheria za nchi .

Aidha ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa miongozo ya utoaji wa maudhui Mtandaoni kwani kufanya hivyo itasaidia kuboresha ustawi wa watoto na jamii yote kwa ujumla.

Ngowi ametaja baadhi ya maudhui yasiyofaa mtandaoni kuwa ni pamoja na picha za ngono, matumizi ya madawa ya kulevya, ukatili wa aina mbalimbali , udhalilishaji na vitisho kwa kutumia picha, kumrubuni mtoto mtandaoni, na mengine mengi.