Chai FM

Jamii iwatembelee watu wenye uhitaji

14 December 2021, 5:14 am

RUNGWE-MBEYA

Wazazi na walezi wameaswa kuwajali  na kuwathamini watu wenye uhitaji kwa kutoa mahitaji muhimu kwa watoto hao ikiwemo kuwatembelea katika maeneo mbalimbali kwani itasaidia kuongeza faraja kwao.

Hayo yamezungumzwa  na Umoja wa akina mama kutoka Katumba walipo watembelea watoto katika Hosptali ya Igogwe  wilayani Rungwe ambapo wamesema ni wakati sasa jamii iweze kuelimika kwa kuwajali watu wenye uhitaji kwa kuwatembelea na kutoa misaada mbalimbali ambayo itawafanya waweze kuepukana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili.

Sista Monika Mandate ni mlezi wa watoto katika kituo hicho nae ameeleza idadi ya watoto ambao wanao katika kituo hicho kuwa ni watoto 37, amesema baadhi ya watoto wamekuwa wakichukuliwa na wazazi wao na wengine  wamekuwa wakitelekezwa na wazazi wao bila msaada na kuwaomba kuacha tabia hiyo kwani inawafanya watoto hao kukosa imani na wazazi wao.

BI.JOYCE  NKEMWA  ambaye ameongoza msafara huo wa akina mama kuwatembelea watoto hao  ameishukuru jamii nzima ya Katumba kwa kushirikiana pamoja na akina mama hao na kuwaomba wasikate tamaa kwani bado wapo wengi wanao hitaji msaada wa jamii.