Chai FM

Zaidi ya watoto elfu 86 kupata chanjo ya polio Rungwe

21 September 2023, 4:40 pm

Mratibu wa chanjo halmashauri ya wilaya ya Rungwe Bw. Ezekiel Mvile akitoa elimu kuhusu chanjo ya polio katika kipindi cha Mtazamo wetu Chai FM (picha na Sabina Martin)

Halmashauri ya wilaya ya Rungwe inatarajia kuwafikia watoto zaidi ya elfu themanini na sita na kuwapatia chanjo ya polio ambayo imezinduliwa rasmi hii leo katika mikoa sita yenye hatari ya kupata ugonjwa huo hapa nchini.

Na Sabina martin – Rungwe
Jamii wilayani Rungwe mkoani Mbeya wametakiwa kutoa ushirikiano kwa watoa huduma wa afya wanaoendelea kutoa chanjo ya polio kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka nane.

Akizungumza katika kipindi cha Mtazamo Wetu kinachorushwa Chai FM mapema leo alhamisi septemba 21. 2023 mratibu wa chanjo wilaya ya Rungwe Bw. Ezekiel Mvile amesema kwamba chanjo hiyo inatolewa bure hivyo ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapatiwa chanjo hiyo.

Mvile amewapongeza wananchi wa wilaya ya Rungwe kwa namna wanavyopokea taarifa za chanjo na kuchukua hatua pale inapobidi ambapo watoto zaidi ya elfu 86 wanatarajiwa kufikiwa.

Katika hatua nyingine Mvile amesema kuwa chanjo ya polio haina madhara kwa mtoto yeyote atakayepatiwa huku akitoa rai kwa jamii kuendelea kuhamasishana watoto kupatiwa chanjo hiyo.

Katika hatua nyingine Mvile ameeleza kwamba mtoto atakayekosa chanjo hiyo yupo kwenye hatari ya kupata ulemavu wa kudumu unaosababishwa na polio.

Chanjo ya polio inatolewa katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa, Kagera na Kigoma kuanzia leo sept 21-24sept 2023 na wizara ya afya kupitia idara ya kinga sehemu ya elimu ya afya kwa umma na mpango wa taifa wa chanjo.