Chai FM

Wananchi waomba kuanzishwa halmashauri mpya Makete

12 December 2023, 1:28 pm

Na Mwandishi wetu – Makete

Wananchi na wadau wa maendeleo wa kata 11 kati ya 23 za halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe wameiomba serikali kuigawa halmashauri hiyo na kuazisha halmashauri mpya kutokana na jiografia ya wilaya hiyo.

Kikao cha kupata maoni ya wadau mbalimbali juu ya kupata halmashauri mpya ya wilaya ambayo wamependekeza kuipa jina la halmashauri ya wilaya kitulo ni kutokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma kutokana na umbali kutoka makao makuu ya halmashauri ya wilaya mama ya Makete.

Wananchi wameiomba selikali kuwepo na halmashauri mbili ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo vyeti ya kuzaliwa, vitambulisho vya NIDA, huduma benki na huduma nyingine za kijamii.

Mwenyekiti wa kikao hicho Bi Rhoda Nsemwa ameiambia Mwananchi kuwa wananchi wasihofu kuhusu vigezo kwa kuwa serikali inaangalia mambo mengi hadi kufikia hatua ya kugawa eneo la kiutawala na kuwa halmashauri ya wilaya.

“Nikiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya kabla sijastaafu nimeshiriki katika michakato ya kuanzishwa kwa halmashauri tatu mpya hivyo ni a uzoefu mkubwa kwenye hatua za kuanzisha Halmashauri mpya ya Wilaya” alisema Bi Nsemwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Makete Clemence Mawite Ngajilo amewaasa wananchi na wadau hao kuwa wasikubali kugawanyika juu ya ombi hilo badala yake amewataka kuwa kitu kimoja katika mchakato huo wa kuiomba serikali kuwepo na halmashauri mbili katika wilaya hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Makete Williamu Makufwe ambaye amekuwa ni mmoja ya washiriki katika kikao hicho, ametoa muongozo wa kufuata katika mchakato wa kuiomba serikali kupitia kwa waziri mwenye dhamana kuhusu ombi la kuazishwa kwa halmashauri mpya.

“Hatua zinazotakiwa kufuatwa ili kukidhi vigezo vya maombi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kitulo na kuwataka wananchi na viongozi kutoa ushirikiano ili kutimiza mahitaji ya jamii ya wakazi wa eneo hili ambao wanapitia changamoto kubwa kupata huduma za misingi kwa kuanzisha halmashauri mpya  kutokana na ugumu ya mawasiliano ya kijiografia katika Wilaya ya Makete” amesema Makufwe

Katibu wa Kamati ya maombi ya Halmashauri ta Wilaya ya Kitulo Valentino Malila amesema wananchi na wadau walishaanza vikao mapema na hiki ni kikao cha tatu na tayari nyaraka mbalimbali zimakamilika nilikupeleka maombi hayo kwenye vikao vya Baraza la Madiwani kwa hatua zaidi.

Mdau wa maendeleo kutoka Makete Bwana Ahadi Mtweve amesema licha ya kuwa na idadi ndogo ya wananchi wakaazi wa eneo linalotarajiwa kuunda Halmashauri ya Wilaya ya Kitulo lakini tumekidhi vigezo vingine ikiwemo makusanyo ya fedha zinazotokana na mapato ya ndani na huduma za jamii huku sababu ya mawasiliano na ugumu wa jiografia ya Wilaya ya Makete ikitajwa kuwa sababu kuu.

Maombi ya Halmashauri ta Wilaya ya Kitulo yanahusisha tarafa za Matamba, Magoma na Ikuwo ambapo jumla ya kata 11 zinazotarajiwa kuundwa kwa halmashauri hiyo ambazo ni Matamba, Kinyika, Itundu, Mlondwe, Kitulo ambazo zipo tarafa ya Matamba. 

Nyingine ni Ikuwo, Mfumbi na Kigala ambazo zinaunda tarafa ya Ikuwo wakati tarafa ya Magoma inaundwa na kata za Ipelele, Iniho na Kigulu.