Chai FM

Usafi kiboko ya magonjwa ya mlipuko

16 December 2022, 12:09 pm

RUNGWE- MBEYA NA: SABINA MARTIN

Msimu huu wa mvua zilizoanza kunyesha wilayani Rungwe mkoani Mbeya wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari na kuzingatia afua za afya ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.

Akizungumza na Chai FM ofisini kwake afisa afya wa wilaya ya Rungwe Bw. Godfrey Kilauwo amesema kwamba ni jukumu la kila mmoja kutunza mazingira kwani wilaya ya Rungwe ni miongoni mwa wilaya zenye muingiliano na nchi jirani ya Malawi ambayo imeripoti uwepo wa ugonjwa huo tangu mwezi agost mwaka huu.

Aidha amesema kwamba ujenzi na matumizi ya vyoo bora ni moja kati ya njia bora za kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama vile kuhara na kipindupindu.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Chai FM wameiomba serikali kupitia idara ya mazingira kuboresha miundombinu ya masoko kama vile mifereji pamoja na vizimba vya kuhifadhia taka ili zisizagae hovyo.

Katika hatua nyingine wananchi hao wameeleza kwamba uhaba wa matundu ya vyoo katika masoko kama vile soko la ndizi la madonde Tukuyu mjini ni changamoto inayofanya baadhi ya wananchi kujisaidia vichakani.