Chai FM

Serikali za vijiji zishiriki elimu chanjo UVIKO

8 November 2021, 7:17 am

RUNGWE-MBEYA

Jamii wilayani Rungwe imeendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Virus vya Corona kwa kuendelea kuzingatia upataji wa chanjo inayoendelea kutolewa kote nchini.

Akizungumza na Radio Chai FM Mwenyekiti wa kitongoji cha Mabonde kata ya Msasani Wilayani Rungwe Ndg.ELIAS  MWASAMBILI amesema kuwa hapo awali wananchi walikuwa wameweka nguvu zaidi katika kuzingatia zile kanuni za afya kujikinga dhidi ya maambukizi ya corona lakini kwa sasa zaidi wananchi wanaendelea kupokea chanjo inayotolewa  katika maeneo yao.

Hata hivyo mwenyekiti MWASAMBILI amesema kama Serikali ya Kijiji na Kitongoji wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na wakuhamasisha wananchi kupata chanjo inayotolewa na serikali kwa hiari.

Sambamba na hilo amewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo na kuondokana na mitazamo potofu kuhusu chanjo huku akisema wao kama viongozi wanaimani na wengi wao tayari wamepata chanjo hiyo.