Chai FM

Wakala afikishwa mahakamani kwa kosa la uhujumu uchumi Rungwe

1 November 2023, 7:51 pm

Na Mwandishi wetu: Rungwe – Mbeya

Wakala wa kukusanya ushuru katika  halmashauri ya wilaya ya Rungwe amefikishwa mahakamani kutokana na kesi ya uhujumu uchumi.

Oktoba 30, 2023 katika Mahakama ya Wilaya Rungwe, mbele ya  Hakimu Mhe. Mwinjuma Bakari Banga  imefunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 04/2023, Jamhuri dhidi ya

Steven Meo Mwasumilwe ambaye ni Wakala wa kukusanya ushuru Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Mshitakiwa huyo ameshtakiwa kwa kosa la kugushi stakabadhi  zenye  kiasi cha Sh. 330,000/= mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.

Ilidaiwa kuwa  Bwana Mwasumilwe alikusanya fedha za Ushuru wa Mazao na kufuja fedha hizo Kwa kutoa stakabadhi za kugushi  baada ya hapo alizitumia  fedha hizo  kwa matumizi yake binafsi. 

Kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 335(a) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16(RE: 2022) Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yake amerudishwa rumande baada ya kukosa dhamana na shauri limepangwa kutajwa tena Novemba 13, 2023 kwa kuwa uchunguzi bado  haujakamilika