Chai FM

Diwani avunja kamati ya shule

11 March 2024, 2:07 pm

Diwani wa kata ya Kijombe Seylvester Kigola akizungumza na wazazi na wananchi wa Kijombe hawapo pichani(Picha na Cleef Mlelwa)

Baada ya wazazi na walezi kuonesha kutokuwa na imani na kamati ya shule imemlazimu diwani kuingilia kati suala hilo.

Na Cleef Mlelwa – Wanging’ombe

Diwani wa kata ya Kijombe Seylvester Kigola ameagiza kuvunjwa kwa kamati ya shule ya msingi Ikwavila na kuchaguliwa nyingine kutokana na ile ya awali kulalamikiwa na wazazi kwa kutosoma taarifa ya mapato na matumizi kwa wakati na kushindwa kusimamia mali za shule.

Akizungumza katika kikao ambacho kimefanyika shuleni hapo,Diwani Kigola amesema kutokana na malalamiko hayo hakuna haja ya kuendelea kuwa na kamati hiyo kwani wazazi hawatakuwa na mwamuko wa kuendelea kufanya shughuli mbalimbali za shule hiyo ikiwemo kutoa michango.

Sauti ya diwani akitoa agizo

Aidha Diwani huyo amewataka wazazi hao kuchagua kamati ya chakula ambayo itasimamia utaratibu wa watoto kupata chakula shule na kulinda mazao yanayotolewa kwaajili ya chakula huku akiwataka kuacha tabia ya kuwaruhusu watoto wao kukaa kwenye kumbi za kuonyeshea mpira usiku.

Sauti ya diwani kuhusu Chakula shuleni

Naye mwenyekiti wa kamati ya shule amesema Joseph Amigo Ng’amilo ameridhishwa na maamuzi ambayo yametolewa na diwani huyo na kueleza kuwa malalamiko hayo yamesababishwa na wajumbe wa kamati hiyo kumwachia majukumuu pekee yake.

Sauti ya mwenyekiti wa kamati ya shule

Hata hivyo mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Ikwavila Samweli Hosia Mdapo amesema atahakikisha uchaguzi wa kuchagua kamati mpya ya shule unafanyika kwa wakati ili kukuza taaluma ya shule hiyo.

Sauti ya mwenyekiti wa kijiji

Nao baadhi wazazi katika kijiji cha Ikwavila,Neema Mfanyakalendi,Faraja Mubanga,Histi Kig’wenyu na Thobias Chavala wamesema changamoto kubwa ni kamati hiyo kushindwa kusimamia vyema shule hiyo kwa kuacha mazao yanayolimwa katika mashamba ya shule kufanyiwa ubadhirifu na kutokuwa na mpishi wa kudumu shuleni hapo na kusababisha wakati mwingine watoto kurudi kula nyumbani licha ya wao kutoa mchango wa chakula.

Sauti za wananchi wa Ikwavila