Chai FM

Halmashauri ya Rungwe imekusanya mapato kwa asilimia 80%

13 February 2022, 1:20 pm

Baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Rungwe limefanya kikao kilichotoa taswira hali ya ukusanyaji mapato huku Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mhe. Mpokigwa Mwankuga akiwataka Madiwani pamoja na watendaji idara mbalimbali kuendeleza juhudi za kusimamia miradi na mapato katika maeneo yao.

Mwenyekiti wa halmashauri akiongoza kikao cha baraza la madiwani

Amebainisha kuwa kwa kipindi cha robo ya pili kuanzia mwezi oktoba mpaka Disemba 2021 Halmashauri imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 1,065,276,135.33 sawa na asilimia 80% ya makisio ya shilingi 1,326,564,689.00.

Aidha kuanzia Julai mpaka Disemba 2021 Halmashauri imekusanya jumla ya Shilingi 2,686,228,943.04 sawa na asilimia 51 ya makisisio ya mwaka ya shilingi 5,306,258,756.00 katika  vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwa ni ushuru wa mazao,leseni na vyanzo vingine.

madiwani wakifuatilia kwa umakini kikao cha baraza

Mwenyekiti wa halmashauri Mh Mpokigwa amesema kuwa Mapato hayo yamesaidia kutanua huduma za kijamiii ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, Ujenzi na ukamilishaji wa zahanati na kituo cha afya Kinyala, urahisishaji Shughuli za utawala na kadhalika.

Naye Mkuu wa wilaya ya Rungwe Dr Vicent Anney amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya afya hivyo watendaji wanawajibu kusimamia miradi ili ikamilike na iweze kuwahudumia wananchi.