Wasichana 21,094 kupatiwa chanjo ya HPV Rungwe
23 April 2024, 4:08 pm
Halmshauri ya wilaya ya Rungwe imekusudia kuwalinda watoto wa kike wenye umri wa kuanzia miaka 9-14 kwa kuwapatia chanjo ya kupambana na saratani ya mlango wa kizazi (HPV)
Na Judith Mwakibibi
Mkuu wa wilaya ya Rungwe Jaffar Haniu amewataka maafisa elimu pamoja na waalimu kwa kushirikiana na wazazi kuhakikisha wasichana wenye umri wa miaka 9-14 wanapata chanjo ya HPV zinazotolewa kwa ajili ya kuwakinga na saratani ya shingo ya kizazi
Haniu ameyasema hayo katika kikao cha kamati ya afya ya msingi halmashauri ya Rungwe kilichofanyika katika ukumbi wa John Mwankenja huku akisema kuwa chanjo hiyo haina madhara kwa wale watakaochanja.
Akitoa ufafanuzi kwa shule ambazo zimeonesha kuto toa ushirikiano kwa wachanjaji mkuu wa wilaya ametaka ofisi ya mganga mkuu kwa kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu kwa wananchi huku akiwataka wakuu wa shule kujua kuwa zoezi hilo ni la kisheria na ni haki ya mtoto kupata kinga.
akisoma taarifa ya maandalizi ya zoezi hilo kaimu mratibu wa chanjo wilaya ya Rungwe Salvatory Shayo amesema kuwa serikali imeamua kutumia dozi moja ambapo wilaya ya Rungwe imekusudia kufikia watoto 21 094 na tayari zoezi hilo limekwishaanza siku tarehe 22 april, 2024.