Chai FM
Chai FM
4 February 2025, 1:19 pm

Katika safari ya kuelekea Tanzania 2050 taasisi zinazohusika na usimamizi wa haki madai ni muhimu zikajikita kutekeleza malengo yaliyoainishwa katika dira ya taifa ya maendeleo.
Na Sabina Martin
Rai imetolewa kwa tume ya kurekebisha sheria Tanzania kufanya utafiti wa kina kabla ya kutunga sheria ili sheria zitakazotungwa na bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania ziendane na maendeleo ya sayansi na Teknolojia kama inavyolengwa na dira ya taifa ya maendeleo 2050.
Ili kufanikisha hayo mwawakili na wanasheria wanatakiwa kujiendeleza kitaaluma na kushiriki mafunzo mbalimbali ili waweze kufanya upekuzi wa mikataba na hati za makubaliano kwa ufasaha.

Hayo yamebainishwa na Bi. Veronica Mtafya mwendesha mashtaka wa wilaya katika maadhimisho ya wiki ya sheria yaliyofanyika februari 3. 2025 katika mahakama ya wilaya ya Rungwe.
Hagai Nelson Sanga ni wakili na mwakilishi wa TLS wilaya ya Rungwe ameeleza kuwa chama cha wanasheria Tanganyika wataendelea kuwasaidia wananchi kupata msaada wa kisheria pamoja na kutekeleza majukumu yao bila uwoga.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya katika maadhimisho hayo Afisa Tawala wa wilaya ya Rungwe Bw. Amimu Mwandelile amesema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama ili kuendeleza utawala wa sheria.
Akihutubia katika sherehe hizo Hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Rungwe Bw. Jackson Thomas amesema ili kuendana na sayansi na teknolojia Mahakama imekua ikisikiliza pia mashauri kwa njia ya kidijitali ili kuepusha kupoteza muda kwa wananchi kufika mahakamani kila wakati.
Maadhimisho ya wiki ya sheria hufanyika kila mwaka nchini Tanzania ambapo maadhimisho ya mwaka huu yalibebwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania 2050 nafasi ya taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia malengo makuu ya dira ya Taifa ya maendeleo”.