Kitulo FM

Kamati ya siasa mkoa Njombe yakagua utekelezaji wa ilani ya CCM Makete

26 August 2026, 9:32 am

Kamati ya Siasa ya  Chama Cha Mapinduzi, CCM, Mkoa wa Njombe wakiwa kwenye ukaguzi wa miradi

kamati ya siasa mkoa wa njombe imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbali mbali ambayo inatekelezwa katika wilaya ya makete kuona kama miradi hiyo imejengwa kulingana na fedha zilizopelekwa ili kuwa na manufaa ya wananchi huku wakisisitiza miradi ambayo bado kukamilika iweze kukamilishwa haraka

na mwandishi wetu.

Kamati ya Siasa ya  Chama Cha Mapinduzi, CCM, Mkoa wa Njombe imefanya ziara ya ukaguzi wa utekelezaji  Ilani ya Chama hicho kwa kutembelea miradi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1,285,800,213 katika Kata za Lupila, Ipepo, Ukwama, Bulongwa, Iwawa na Ipelele Wilayani Makete.

Kamati ambayo imeongozwa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi,  mkoa wa Njombe, Ndg. Julius Peter, imekagua ujenzi na ukamilishaji wa madarasa, miundombinu ya maji na usafi wa mazingira (WASH), matundu ya vyoo, majengo ya hospitali, pamoja na vichomea taka, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya na elimu kwa wananchi.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Ndg. Julius Peter, amesema wananchi wanapaswa kuona umuhimu wa miundombinu hiyo kwa kuhakikisha kuwa wanaitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu, katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

baadhi ya wananchi wakiwa kwenye mkutano wa kamati hiyo ya siasa

Sambamba na hayo, Kamati hiyo ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi, imesisitiza ukamilishaji wa haraka kwenye miradi ambayo bado inajengwa ili wananchi waanze kuona manufaa ya Serikali inayoongozwa na CCM.

hata hivyo Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi, CCM, Mkoa wa Njombe jana Agosti 25, 2026, imehitimisha   ziara yake ya siku ya pili ya Ukaguzi wa Utekelezaji wa Ilani ya CCM, kwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo  yenye thamani ya Shilingi Milioni 799,233,690 katika Kata za Kipagalo,  Luwumbu, Mfumbi na Itundu,lpepo.

Kamati hiyo, ya Siasa ya CCM, ikiwa imeongozwa na Katibu wa Chama hicho mkoa wa Njombe, Ndg. Julius Peter,  imesema kuw imeridhishwa na Utekelezaji wa Ilani ya Chama, na kusisitiza umuhimu wa wananchi na watumiaji wa miundombinu hiyo kuitunza na kuilinda ili iweze kutoa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu na kuhakikisha thamani ya fedha za Serikali inalindwa.

Sambamaba na hayo, Kamati hiyo, imewataka wananchi kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano, kwakuwa ndio msingi wa maendeleo katika kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi.

Ikumbukwe kuwa ziara hiyo ya Kamati ya Siasa imefanya ziara ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama katika Kata za Lupila, Bulongwa, Ipelele, Ipepo, Ukwama, Iwawa, Lupila, Mfumbi, Itundu, Kipagalo na Luwumbu, ambapo miradi yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 2, imekaguliwa.