Kitulo FM

Milioni 170 kujenga Daraja Kijiji cha Makwaranga-Makete

December 29, 2022, 7:54 am

Daraja linalojengwa kuunganisha kijiji cha Makwaranga na Ipelele

Serikali imeanza ujenzi wa Daraja la Zege litakalounganisha Kijiji cha Ipelele na Makwaranga Kata ya Ipelele Wilaya ya Makete lenye thamani ya zaidi ya Milioni 170.

Daraja hilo litawafanya wananchi wa vijiji hivyo kutumia barabara ya Ipelele-Makwaranga yenye urefu wa zaidi ya Km 5 kuwasaidia kufanya shughuli zao za usafirishaji mazao kwa urahisi tofauti na ilivyo sasa ambapo wananchi hao wanatumia daraja la Mbao.

Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Makete John Peter Kawogo amesema tayari ujenzi umeanza na baada ya miezi miwili ijayo Daraja hilo linaweza kuwa limekamilika kutegemeana na hali ya mvua inanyesha Wilayani Makete.

Mbunge wa Jimbo la Makete Mhe. Festo Sanga akiwa kwenye Mkutano na wananchi wa Kijiji cha Makwaranga amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa Barabara hiyo na ukuaji wa uchumi imeamua kuwekeza fedha nyingi ili kujenga daraja la Uhakika.

Shadrack Sanga na Maria Sanga Wananchi wa Kijiji cha Makwaranga wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Daraja hilo muhimu huku wakiomba kujenga barabara kwa kiwango cha kokoto eneo lenye mlima mkali wenye urefu wa Kilomita 1.5 ili kurahisha zaidi usafirishaji wa mazao.

Wananchi wa Vijiji vya Ipelele na Makwaranga ni wakulima wa zao la Viazi kwa wingi na Pareto lakini wanalazimika kusafirisha mazao yao kwa kutumia punda au pikipiki (bodaboda) kwa gharama kubwa.