Kitulo FM

Makete kutumia shilingi bilioni nne miradi ya maendeleo

October 9, 2023, 4:47 pm

Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya Makete Bw. William Makufwe akizungumza na wananchi kupitia Morning Power ya Kitulo Fm. Picha na Ombeni Mgongolwa

Kutokana na chanagamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa wilaya ya Makete hususani katika miundombinu ya sekta za elimu, afya, kilimo na ujenzi serikali imetoa fedha zaidi ya bilioni 4 kutatua changamoto hizo.

Na Aldo Sanga

Zaidi ya bilioni nne (Tsh. 4,489,684.61) zimetolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maaendeleo katika halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Fedha hizo zimetolewa na serikali kwa lengo la kuunga mkono juhudi za wananchi katika kuwaletea maendeleo hususani katika sekta ya afya na elimu.

Akizungumza na wananchi kupitia Redio Kitulo Fm mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Makete Bw. William Makufwe ametaja baadhi ya maeneo yaliyoanza utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa makao makuu ya halmashauri ambapo kiasi cha shilingi bilioni moja (1) kimetolewa kuendeleza ujenzi jengo la ofisi huku kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa majengo katika hospitali ya wilaya.

Sauti ya Mkurugenzi mtendaji Makete Bw,William Makufwe

Aidha fedha zingine zimeelekezwa kutekeleza miradi ya madarasa na matundu ya vyoo kwa upande wa elimu huku fedha zingine zikielekezwa katika ujenzi wa vituo vya afya katika kata za Lupalilo, Matamba, Bulongwa pamoja na zahanati.

Wilaya ya Makete inakabiliwa na changomoto ya hali ya hewa ambapo kwa muda wa miezi 7 ni kipindi cha masika huku miezi mitano pekee ikiwa msimu wa kiangazi hivyo kwa wale waliopewa dhamana ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na watendaji na wananchi wametakiwa kutekeleza miradi kwa wakati ili kuikabili changamoto hiyo.