Kitulo FM

Wananchi Makete washauriwa kulima mazao mchanganyiko kukabili baa la njaa

January 31, 2024, 5:11 pm

Dc Sweda akimsikiliza afisa kilimo na mwandishi wetu

Kutokana na wananchi kuhamasika katika kilimo cha kibiashara hususani katika zao la viazi Dc Sweda ametoa tahadhari kwa wakulima wa Makete kulima mazao mchanganyiko ili kukabili baa la njaa baada ya wananchi kujikita zaidi katika zao la viazi pekee.

na Mwandishi wetu

Wananchi wa Kata za Mlondwe na Itundu zilizopo wilayani Makete mkoani Njombe Januari 30, 2024 wemeshauriwa kulima mazao ya aina mbalimbali ya chakula ili kuepukana na njaa pamoja na kujikwamua kiuchumi kotokana na wananchi wa maeneo hayo kulima kwa wingi zao moja la kibiashara (Viazi Mviringo).

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda, akiwa kwenye mkutano wa hadhara ambao umefanyika katika kata hizo mbili za Mlondwe na Itundu, wakati akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kugundua kuwa wananchi hao wamekuwa wakilima zao moja tu la biashara na kupelekea kukosa chakula Kwa msimu wote.

Aidha Mhe. Sweda, amewataka wananchi hao kulima Ngano kwa wingi kwani tayari Serikali imeshatoa mbegu bure kwa kwa ajili ya wakulima ambao watakuwa tayari kulima zao hilo, ambapo Kata ya Mlondwe imeshapata tani 14 za mbegu hizo kwa ajili ya msimu mpya wa Kilimo.

Dc Sweda akiwa katika moja ya miradi ya maendeleo iliyokamilika ikiwemo maabala katika shule ya Secondari Mlondwe

Kwa Upande Afisa Kilimo, wa Kata ya Mlondwe Bw. William Lupenza, ameishukuru Serikali kwa kutoa bure mbegu hizo, na kwamba tayari wameshaanza kufanya mikutano ya hadhara na wananchi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima, ya namna bora ya kulima zao hilo muhimu la kibiashara ili waweze kulima kitaalamu.

Nao, Baadhi ya wananchi wa Kata hizo, wamemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Juma Sweda, kwa kuwatembelea na kusikiliza kero zao pamoja na kuzitatua, ikiwemo ubovu wa barabara kwenye maeneo hayo huku wakisema wapo tayari kwa kilimo cha Ngano na wamewaomba maafisa kilimo kuendelea kutoa elimu ya kilimo hicho ili waweze kunufaika nacho .

Ikumbukwe kuwa, Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda bado anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo inayotekelezwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Makete na katika ziara hizo anawasihi wananchi kushirikiana na Serikali katika shughuli mbalimbali za Maendeleo