Makabidhiano ya Pikipiki kwa Watendaji
Kitulo FM

Watendaji wa Kata wapata Pikipiki 10 H/w Makete

August 26, 2023, 12:52 pm

Halmashauri ya Wilaya ya Makete imekabidhi pikipiki 10 kwa Watendaji wa Kata 10 ili kuboresha ukusanyaji wa mapato kwenye Kata zao.

Akizungumza katika makabidhiano hayo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Mhe. Hawa Kader amesema kuwa, pikipiki hizo zikatumike sawa na mategemeo ya Halmashauri na si vinginevyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Ndg. Willium Makufwe amesema kuwa pikipiki hizo zimenunuliwa ili zisaidie kukusanya mapato na si kufanyia shughuli binafsi kama vile kupakia abiria.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa pikipiki hizo watendaji Kata akiwemo Bi. Rahabu Kibona na Bw. Isaya Kibona wameishukuru Serikali kwa kuwapatia pikipiki hizo kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa ya miundombinu ya usafiri kama vile barabara.

Ikumbukwe kuwa Pikipiki hizo 10 zimenunuliwa kutokana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Ndg. Willium Makufwe kupunguza gharama za manunuzi ya gari la mkurugenzi ili pesa inayobaki iweze kununua pikipiki zitakazo wasaidia watendaji kata kukusanya mapato.

Hii ni awamu ya pili ya ugawaji Pikipiki 10 zenye thamani ya Zaidi ya shilingi Milioni thelathini ambapo awamu ya kwanza zilitolewa pikipiki 7.