Kitulo FM

DC Sweda akasirishwa kituo cha afya kutofanya huduma za upasuaji

October 5, 2023, 8:39 am

DC Samweli Sweda akiwa katika chumba cha upasuaji na timu yake.picha na Furahisha Nundu

Kituo cha afya Lupila kwa muda mrefu sasa kimeshindwa kutoa huduma za upasuaji sababu zikiwa ni kukosekana kwa mtaalam wa upasuaji na kupelekea adha kubwa kwa wananchi wanaolazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya kilomita zaidi ya 50 hadi Ikonda.

Na Furahisha Nundu

Baada ya wananchi wa kata ya Lupila kuibua changamoto ya ukosefu wa huduma ndogondogo za upasuaji kutofanyika kituo cha afya Lupila, mkuu wa wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda ameonesha kukasirishwa na kitendo cha kukosekana kwa huduma hiyo kwa miaka minne ilihali vifaa vipo.

Mh. Sweda amemtaka Mganga Mkuu atoe maelezo ya kutosheleza kuhusu huduma kukosekana kituoni hapo, vifaa vimeletwa miaka minne iliyopita, jengo zuri lipo kwa nini hawatoi huduma na serikali imeleta mtaalam wa usingizi lakini hakuna huduma.

Wakizungumza mbele ya mkuu wa wilaya baadhi ya wananchi akiwemo diwani wa Viti Maalum tarafa ya Ukwama Bi. Elenesta Ngwata wameshukuru serikali kwa kutembelea miradi na kujionea hali halisi ya miradi. Mkazi mmoja wa kijiji cha Malanduku Bi. Tweve amemwambia mkuu wa wilaya kuwa wanakosa huduma ya upasuaji mdogo kwenye kituo hicho na kulazimika kufuata huduma hospitali ya Ikonda umbali wa zaidi ya kilomita 60.

Diwani viti maalum akizungumza mbele ya DC. Picha na Furahisha Nundu

Wakati huohuo wananchi wamemwomba mkuu wa wilaya kuletewa gari la kubeba wagonjwa (Ambulance) kwani wamekuwa wakitumia gharama kubwa kukodi magari binafsi.