Mkuu wa Wilaya akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ikuwo
Kitulo FM

Makete: Zaidi ya shilingi mil. 300 kujenga shule ya msingi Ighala-Ikuwo

June 8, 2023, 2:26 pm

Mkuu wa wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda amesema serikali ya awamu ya sita imetoa fedha zaidi ya shilingi Milioni 347 kupitia mradi wa BOOST kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi Ighala iliyopo kata ya Ikuwo kijiji cha Ikuwo.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kupunguza adha ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kufuata elimu badala yake wapate elimu karibu na makazi yao.

Pia Mhe. Sweda amewasihi wananchi wa Ikuwo kuwa walinzi wa vifaa na wasimamizi wa kwanza wakati wote wa ujenzi wa shule hiyo na kuachana na tabia ya wizi ambayo imeshuhudiwa katika miradi mingi ya Serikali inayotekelezwa kwenye maeneo yao.

Veronica Mbwilo na Yusti Ng’wavi wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wote kwa kuwapelekea mradi huo mkubwa ambao hawakutarajia kama wangepata madarasa katika eneo hilo waliloanza kujenga vyumba viwili ya madarasa

Flora Mbwilo M/kiti wa kijiji cha Ikuwo ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha kujenga shule ya msingi Ighala na kuongeza kuwa imekuwa neema kwa wananchi wa Ikuwo na kuwapunguzia safari ndefu wanafunzi.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Makete William Makufwe amesema Halmashauri ya imepokea zaidi ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule ya Ighala, Kinyika, Missiwa na Mlanda.