Kitulo FM

Elimu ya Upimaji Ardhi yawakomboa Wananchi

September 27, 2023, 7:51 am

Zoezi la Upimaji vipande vya Ardhi likiendelea. Picha na Furahisha Nundu

Katika kuhakikisha Wananchi wanapata Hatimiliki za Ardhi,Serikali imechukua hatua za kupima na kugawa Hatimiliki bure kwa Wananchi

Na Furahisha Nundu

Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi umeendelea kufanyika ambapo Wananchi wa Kijiji cha Malanduku Wilayani Makete wameonesha njia bora ya kutatua migogoro kwa njia rahisi yenye kuleta tija kila upande.

Hatua hiyo imeshuhudiwa baada ya Wizara ya Ardhi, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kufika kijijini hapo na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa Wananchi kumiliki Hatimiliki ya Ardhi ambayo itasaidia kupunguza Migogoro isiyokuwa na tija kwa Wananchi.

Sauti za Wananchi na Viongozi wakitatua migogoro ya Ardhi kwa njia ya makubaliano

Happy Sanga na Adophina Lwila ni wakazi wa Kijiji hicho wameishukuru Serikali kwa kupima arhi jambalo ambalo hawajawahi kufikiria hapo awali kwamba watakuja kumiliki Hati ya Ardhi.

Edward Mwaigombe Afisa Ardhi (W) Makete amesema mashamba zaidi ya 500 yanatarajiwa kupimwa na kugawiwa Hatimiliki kwa wananchi wa Kijiji cha Malanduku Wilayani Makete Mkoani Njombe

Dkt. Charles Mkalawa kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi amesema Wizara kwa kushirikiana na Wadau ambao ni kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Benki ya Maendeleo ya Afrika wameanza zoezi la upimaji wa vipande vya Ardhi (Mashamba) yanayomilikiwa na Wananchi ili waweze kupata Hatimiliki bila gharama yoyote na waweze kukuza shughuli za Uchumi kwa Mwananchi mmoja mmoja kwa ajili ya uwekezaji

Mnamo mwezi Juni zoezi la Upimaji Ardhi na ugawaji wa Hati za HakiMiliki za Kimila lilianza kufanyika katika Vijiji 44 kati ya 64 Wilayani hapa, ambapo sasa zoezi hilo limeanza awamu ya Pili katika Vijiji 20 kutoka Kata mbalimbali ikiwemo Kata ya Lupila

Mtaalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (Madam Pili) akizungumza na Wananchi. Picha na Furahisha Nundu