Kitulo FM

Milioni 200 Kujenga Mradi wa Maji Kijiji cha Tandala Wilayani Makete

December 30, 2022, 8:08 pm

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga

 

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Antoni Sanga amesema Serikali imetoa fedha Milioni 200 kukabiliana na uhaba wa Maji kijiji cha Tandala Kata ya Tandala Wilayani Makete.

Mhandisi Sanga leo amefika Tandala na kukutana na viongozi wa Kijiji ambapo amesema fedha hizo zitaondoa tatizo la Maji kwa wananchi wa vitongoji vya Posta na Singida ambao wamekuwa wakipata maji kwa Mgao na kusisitiza kuwa Tandala inapaswa kupata maji kwa 100% na siyo asilimia 80 au 90.

Katibu Mkuu huyo amewasisitiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Makete (RUWASA) kuhakikisha mradi huo wa ujenzi wa Chanzo cha maji na usambazaji mabomba unafanyika kwa kipindi cha miezi minne kuanzia Januari 2023 hadi Aprili 2023 wananchi waanze kupata huduma hiyo huku akiahidi kuwa Serikali itatoa Dira 100 ili kuanza zoezi la ufungaji wa Dira hizo kwenye makazi ya watu.

Awali Kaimu Meneja wa RUWASA Makete Martin Luvanda ameeleza namna ambavyo RUWASA wanaweza kujipanga kukabiliana na uhaba wa Maji Kijiji cha Tandala kwa ujenzi wa Chanzo, kufanya ukarabati wa miundombinu iliyopo na wamepanga kununua dira 500 za Maji ili kuzifunga kwenye makazi ya watu

Wananchi wa Kijiji cha Tandala Chesko Kitumbika Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji Tandala na Maulisia Sanga wameeleza adha wanayokutana nayo hivi sasa kufuatia kupata maji kwa Mgao huku wakiishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo Milioni 200 ili kusaidia upatikanaji wa huduma hiyo muhimu isiyokuwa na mbadala

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Yusuph Ilomo ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo ili kukabiliana na uhaba wa Maji katika kijiji hicho, huku akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi pindi itakapotangazwa kusaidia shughuli mbalimbali ikiwemo uchimbaji wa Mitaro, usogezaji bomba n.k