Kitulo FM
Kitulo FM
11 June 2026, 9:56 am

Lulu Samson pamoja na mganga Mfawidhi hospitali ya wilaya ya Makete Dkt Amanda Mollel
Jamii imesisitizwa kuendelea kuyakumbuka makundi maalumu katika maeneo yao ili kuwafariji na kuwapa pole ili waweze kupata faraja kutoka kwa watu wengine wanaowatembelea
Na mwandishi wetu.
Jamii imeshauriwa kuona umuhimu wa kuwatembelea makundi yenye uhitaji yakiwemo watoto na wanawake wajawazito kwa kuwa ni miongoni mwa makundi yanayohitaji faraja lakini pia kusaidiwa kwa kadri mtu atakavyojaliwa
Rai hiyo imetolewa na mwanahabari Lulu Samson wa kituo cha redio Kitulo FM muda mchache baada ya kutembelea wanawake wajawazito pamoja na watoto waliozaliwa na wanaoendelea kupata huduma za kiafya katika hospitali ya wilaya ya Makete na kutoa zawadi mbalimbali kwao

Lulu amesema yeye ni miongoni mwa waliopitia katika hali hiyo katika maisha yake na kumshukuru Mungu hapo alipomfikisha hivyo akaona ni vema kwenda kuwatembelea wanawake wajawazito, watoto waliozaliwa kwa wakati pamoja na wale waliozaliwa kabla ya wakati

Baadhi ya uongozi wa hospitali na mwanahabari wakati wa utoaji wa baadhi ya vitu kwa wagonjwa
Amewashukuru marafiki zake waliomuunga mkono kwenye wazo hilo kwa hali na mali ikiwemo kuongezea vitu alivyokuwa amekwisha vinunua awali, na wengine walioongozana naye kwenda hospitalini hapo kuvikabidhi
Dkt Amanda Mollel ni Mganga Mfawidhi hospitali ya wilaya ya Makete ameelezea furaha yake kwa kitendo hicho na kuwaomba wadau wengine kuiga mfano kwa kuwatembelea wagonjwa na wote wenye uhitaji

Mwanahabari Lulu Samson wa kituo cha redio Kitulo FM akikabidhi vitu mbali mbali
Wagonjwa waliopewa vitu hivyo wameshukuru kwa kukumbukwa na kumuombea heri mwanahabari Lulu na kusema jambo hilo limewasaidia pakubwa katika kipindi hiki wanachoendelea kupokea matibabu hospitalini
Makundi hayo yamekabidhiwa vitu mbalimbali ambavyo ni, sabuni, mafuta ya kupakaa, taulo za kike, pamoja na pampasi za watoto.