Kitulo FM

Shule ya sekondari Lupila wilayani Makete yakabidhiwa vitabu

October 18, 2023, 12:56 am

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi na mdau wa Maendeleo Wilaya ya Makete Ndg. Antony Sanga akikabidhi Vitabu kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na mdau wa maendeleo wilaya ya Makete Ndg. Antony Sanga amekabidhi vitabu vya kiada vyenye thamani ya shilingi milioni saba laki tisa na elfu themanini shule ya sekondari Lupila wilayani Makete mkoani Njombe.

Akiwa kwenye sherehe za mahafali ya 32 ya kidato cha nne shuleni hapo Oktoba 13, 2023 Sanga amekabidhi vitabu hivyo vilivyotolewa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa niaba ya wadau wengine wa maendeleo wilayani Makete ambapo amesema sasa ni kazi kwa walimu na wanafunzi kuvitumia vitabu hivyo kwani Vitabu vyote vilivyoombwa vimekwisha letwa.

Kuhusu changamoto ya umeme kutofika katika shule hiyo amesema wataendelea kulishughulikia suala hilo sambamba na changamoto ya Barabara ya Lupila-Kipengere ili kuwapunguzia adha wananchi wa ukanda huo hasa wanafunzi wanaosoma Lupila Sekondari.

Daniel Okoka ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo amewapongeza wadau wa Maendeleo pamoja na Serikali kwa mchango wao mkubwa katika shule hiyo.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Abkasa John Ngwale amesema baada ya kupata vitabu hivyo kutawaongezea ufanisi kwenye ufundishaji ukilinganisha na hapo awali.

Furaha Godbles Fungo pamoja na Willis Sahali kwa niaba ya wazazi wa wahitimu wa kidato cha nne wamewasihi watoto hao kwenda kuzingatia waliofundishwa na walimu wao katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne ili watimize malengo yao.

Baadhi ya wahitimu waliozungumza na Green fm wamesema wamejiandaa kufanya vizuri kwenye mtihani wao unaotarajiwa kuanza Novemba 13,2023.