Elimu ya Lishe ikitolewa kwa wazazi na walezi Kijiji cha Maleutsi
Kitulo FM

Wito: Wanaume ongozaneni na wenzi wenu kliniki

June 23, 2023, 12:59 pm

Wanawake Kijiji cha Maleutsi Kata ya Iwawa Wilaya ya Makete wameaswa kuongozana na waume zao kwenda Kliniki ya kwanza wanapohisi kuwa wajawazito.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Lishe Wilaya ya Makete Bi. Jackline Nanauka akiwa kwenye maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe yaliyofanyika leo Juni 23, 2023 kijiji cha Maleutsi

Nanauka amesema ni muhimu kwa Wanaume kwenda Kliniki ya kwanza ya ujauzito wakiwa wameongozana na wenza wao ili kupata elimu ya pamoja namna ya kumtunza mwanamke mjamzito na mtoto mdogo.

Nanauka akiwa kwenye maadhimisho hayo ya siku ya Afya na Lishe Kijiji cha Maleutsi amefundisha namna ambavyo wazazi na walezi wanapaswa kuwalisha vyakula vyenye lishe watoto waliochini ya miaka mitano

Pia zoezi la utoaji wa matone ya Vitamini A limefanyika kwa watoto sambamba na upimaji wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi

Siku ya Afya na Lishe hufanyika kila Kijiji katika kila robo ya mwaka ambapo wiki hii Kijiji cha Ihela, Ndulamo na Maleutsi wamefanya maadhimisho hayo kwa nyakati tofauti kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata Afya bora na wazazi na walezi wanazingatia mlo kamili.