Kitulo FM

DC Kissa aipongeza halmashauri ya makete kwa mafanikio ya afua za lishe

29 July 2026, 7:50 pm

Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa

wito umetolewa kwa watendaji wa kata zote ishirini na tatu wilaya ya makete kuhakikisha watoto wanapata chakula mara mbili tofauti na ilivyo kwasasa wanapata chakula mara moja huku akisisitiza jambo hilo litasaidia ufaulu mzuri kwa wanafunzi pamoja na kuendela kukabiliana na utapiamlo

na mwandishi wetu.

Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa, amewaagiza watendaji wa Kata kuhakikisha kuwa Shule zote za Msingi zinapata Chakula mara mbili kwa Siku, ili waweze kuwa na Afya pamoja na kuongezeka kwa Ufaulu wa wanafunzi katika masomo yao.

Mhe. Kissa Kasongwa, amesema hayo wakati wa kikao cha Tathmnini ya Mkataba wa Lishe kwa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, kilichoketi leo Julai 29,2026, katika Ukumbi wa Bomani, ambapo amewasihi watendaji hao pamoja na Idara za Elimu Msingi na Sekondari kuhakikisha kuwa chakula kinakuwepo mashuleni chenye virutubishi vya Lishe bora.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Makete, Bi. Grace Mgeni

Aidha, Mhe. Kasongwa, amepongeza Juhudi za Halmashauri ya Wilaya ya Makete, kwa kuendelea kuwa kinara katika kupambana na Udumavu, kupitia utekelezaji wa Afua mbalimbali za Lishe, sambambana na kuwataka kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa Majukumu yao ya kila siku yahusuyo Lishe.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Mhe. Rabson Mahenge, amewataka wananchi kuwa na utaratibu mzuri wa kula vyakula ili wawe na Afya bora, sambamba na kuhakikisha wanafunzi katika Shule za Msingi na Sekondari, wanapata chakula mara mbili kwa siku kwakuwa itawaongezea afya na ufaulu mzuri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Ndg, Jerry Daimon Mwaga

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Makete, Bi. Grace Mgeni, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, kwa kuhakikisha kuwa Fedha zote ambazo zimetengwa kwa ajili ya Utekelezaji wa Afua za Lishe zinatoka kwa wakati na kupelekea Halmashauri kufanikisha utekelezaji wake.

Sambamba na hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Ndg, Jerry Daimon Mwaga, amesema kuwa kuna haja ya kufanya tathmini ya siku ya SALIKI kupitia kwa Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii, pamoja na ununzi wa Mashine nyingine za kuongeza viini lishe kwenye Unga, pamoja na usimamizi mzuri wa miradi ambayo imeanzishwa na Halmashauri.

baadhi ya wakuu wa idara na watendaji wa kata kwenye kikao cha tathimini ya lishe

Ikumbukwe kuwa, Kila robo Halmashauri ya Wilaya ya Maketem hufanya kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe kwa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, ambapo kwa mwaka huu wa mpya wa Fedha 2026/2027, kikao hicho kitakuwa kinafanyika mara mbili kwa Mwaka.