Chai FM

Aliyechoma picha ya rais ahukumiwa

4 July 2024, 4:49 pm

Mshtakiwa Shadrack Yusuph Chaula akielekea Mahakamani chini ya uangalizi wa polisi

“Kwakua umeshindwa kutetea taifa lako lisiathirike na ushoga hii video inakuhusu wewe na si mtu mwingine”

Na Sabina Martin – Rungwe

Mahakama ya wilaya ya Rungwe mapema leo julai 4. 2024 imemtia hatiani Bw. Shedrack Yusuph Chaula mwenye umri wa miaka 24 kutumikia kifungo cha miaka miwili (2) gerezani au kulipa faini ya shilingi millioni 5 kwa kosa la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandaoni 2015.

Akisoma hati ya mashtaka mwendesha mashtaka wa serikali Rosemary Mgenyi mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya wilaya ya Rungwe Mh. Ramla Shehagiro ameeleza kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo 22/6/2024 katika kijiji cha Ntokela wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Mshtakiwa Shedrack Yusuph Chaula akisubiri kuingia mahakamani chini ya uangalizi wa polisi

Imeelezwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka kuwa mshtakiwa huyo akiwa dukani kwake maeneo ya Ntokela alirekodi ujumbe wa video wenye maneno“Kwakua umeshindwa kutetea taifa lako lisiathirike na ushoga hii video inakuhusu wewe na si mtu mwingine” ikiwa ni taarifa za uongo zenye kupotosha jamii.

Alipopewa nafasi ya kujitetea mahakamani hapo mtuhumiwa huyo Bw. Shadrack Chaula mkazi wa Ntokela amesema yupo tayari kutumikia adhabu yoyote atakayopewa na mahakama hiyo.

Upande wa jamhuri ukiongozwa na mawakili wa serikali Veronica Mtafya na Rosemary Mgeniji umeiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine kwani kitendo hicho kimetafsiriwa kama upotoshaji wa umma, uchochezi unaosababisha uvunjifu wa amani na udhalilishaji.

Akitoa hukumu hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya wilaya ya Rungwe Ramla Shehagiro amesema kwa mujibu wa sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 kifungu cha 16 amemtia hatiani kwenda gerezani kutumikia kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya shilingi milioni tano.

Mshtakiwa Shadrack katika gari ya polisi tayari kupelekwa gerezani

Hata hivyo mtuhumiwa amepelekwa gerezani kwenda kutumikia kifungo baada ya kushindwa kulipa faini.