Elimu ya malezi mwarobaini wa vitendo vya ukatili Makambako
8 March 2024, 8:28 am
Ili kukabiliana na vitendo vya ukatili katika jamii imeelezwa kwamba elimu ya malezi na makuzi kwa wazazi, walezi na watoto ni muhimu ikaendelea kutolewa
Na Cleef Mlelwa – Makambako
Wazazi na walezi katika halmashauri ya mji wa Makambako wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bila kujali jinsia zao.
Wito huo umetolewa na mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii katika halmashauri ya mji wa Makambako Zuena Ungele, akiwa katika shule ya sekondari Deo Sanga wakati akitoa elimu ya kukabiliana na ukatili kwa wanafunzi.
Ungele amesema licha ya wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya darasani bado wanawajibu wa kutoa elimu ya malezi ambayo itawasaidia kukabiliana na vitendo vya ukatili.
Aidha afisa maendeleo ya jamii Scolastika Kasungu amewataka wazazi kutoa chakula bora kwa watoto wao ili kukabiliaba na changamoto ya udumavu.
Naye mwalimu wa shule ya sekondari Deo Sanga Upendo Mapunda amesema kuna umuhimu wa elimu hiyo kuendelea kutolewa kwa wanafunzi hao ili watambue haki zao.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Teopista John, Gloria Kajogoo, Elbon Ngailo, na Justin Mponzi, wamesema bado kuna changamoto ya baadhi ya wazizi kutowasomesha watoto wa kike na kueleza kuwa endapo wote watapewa elimu itasaidia kupunguza mimba za utotoni zinazokatisha ndoto baadhi yao.