Chai yenye ubora chachu ongezeko la bei
16 November 2023, 1:08 pm
Imetajwa kuwa ongezeko la bei ya chai sokoni inategemea ubora wa majani mabichi ya chai kwani huzalisha majani makavu yenye kiwango kizuri hali inayopelekea kuuzwa kwa bei nzuri katika soko la kimataifa.
Na Sabina Martin: Rungwe-Mbeya
Kufuatia kuzinduliwa kwa mnada wa chai kwa mara ya kwanza hapa nchini, mtendaji mkuu wa RBTC –JE Bw. Lebi Gabriel ametoa rai kwa wakulima wadogo wa chai halmashauri za wilaya ya Rungwe na Busokelo kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kuzalisha chai yenye ubora.
Bw. Lebi amebainisha hayo alipokuwa akizungumza kupitia kituo cha radio chai FM amesema kuwa ili kuwa na soko la uhakiki pamoja na kuongeza uzalishaji wa chai iliyo bora ni lazima mkulima azingatie maelekezo ya wataalam ili kufikia kiwako cha juu cha uzalishaji wa majani mabichi.
Ametaja baadhi ya faida atakazo zipatamkulima mdogo kupitia uwepo wa mnada wa chai Tanzania ikiwa ni pamoja na kushawishi wakulima kumiliki viwanda vyao kutokana na umuhimu wa umiliki wa majani makavu sokoni.
Kuhusu mnada kufanyika jijini Dar es salaam badala ya maeneo yanayolima chai mtendaji mkuu huyo wa RBTC-JE amesema urahisi wa usafirishaji nin moja kati ya sababu zilizopelekea serikali kuweka mnada katika jiji hilo la kibiashara hali inayovutia wanunuzi zaidi.
Ikumbukwe kuwa Tanzania kwa mara ya kwanza imezindua mnada wa kununua chai katika jiji la Dar es salaam jumatatu ya novemba 13. 2023 ambapo kabla ya mnada huo chai ya Tanzania ilipelekwa katika mnada wa Mombasa nchini Kenya.