TARURA Rungwe yatakiwa kuboresha barabara za vijijini zipitike kipindi chote
16 November 2023, 12:24 pm
Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini TARURA katika wilaya ya Rungwe wametakiwa kujenga miundombinu ya barabara za vijijini ili zipitike wakati wote hususani wakati wa mvua ili kurahisisha usafirishaji wa majani mabichi ya chai kutoka shambani hadi kiwandani.
Hayo yamejiri katika mkutano mkuu wa Rungwe Skimu Amcos kupitia taarifa ya mwenyekiti wa Amcos hiyo Bw. Robert Mwanyumba.
Taarifa iliyosomwa katika mkutano huo na meneja wa Amcos Bw. Steven Mwaikuka imeeleza kuwa changamoto ya miundombinu inapelekea ucheleweshaji wa chai kufika kiwandani kutokana na ubovu wa barabara hizo.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa miongoni mwa changamoto zingine wanazo kumbana nazo ni pamoja na muamko mdogo wa wakulima kuanzisha mashamba mapya ya chai, malipo ya chai kutolipwa kwa kwa wakati pamoja na baadhi ya wakulima kung’oa miche ya chai kwaajili ya kupanda mazao mengine.
Baadhi ya wakulima katika mkutano huo wametoa rai kwa viongozi wao kuwahisha pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na madawa kwa wakati ili kuongeza tija ya uzalishaji wa majani mabichi ya chai.
Akitolea ufafanuzi kuhusu uagizaji wa mbolea kwa niaba ya mtendaji mkuu wa RBTCJE Bw. Lebi Gabriel, afisa uhusiano na mahusiano wa RBTC Bw. Michael Mbasyula amesema kuwa hadi sasa mchakato unaendelea ili kupata mbolea kwa mfumo wa ruzuku ya serikali kupitia makampuni ya mbolea.
Mkutano mkuu wa Rungwe skim amcos ni mkutano wa kisheria uliofanyika mapema leo ukiwa na lengo la kujenga uShirika wa wakulima wadogo wa chai katika amcos hiyo huku wakulima wadogo wa chai wilaya ya Rungwe wakiwa na kauli mbiu ya chai yako tunza ikutunze msimamo daima.