Rungwe yakabiliwa na udumavu kwa asilimia 26.5
25 October 2023, 10:06 am
Ulaji wa chakula usiozingatia lishe bora umetajwa kuwa sababu inayochangia udumavu kwa watoto wengi wilayani Rungwe.
Na Lennox Mwamakula, Rungwe
Imeelezwa kuwa halmashauri ya wilaya ya Rungwe inakabiliwa na kiwango cha udumavu kwa asilimia 26.5 huku sababu ikitajwa kuwa ni baadhi ya wazazi na walezi kutozingatia lishe bora kwa watoto wao.
Kauli hiyo imetolewa na afisa lishe halmashauri ya Rungwe Bi. Halima Kameta kwenye kipindi cha amka na Chai kinachorushwa Chai FM ambapo amesema kutokana na tabia ya jamii kula chakula cha aina moja inasababisha kuwepo kwa changamoto nyingi kwenye hatua ya ukuaji.
Aidha Bi Kameta amesema kuwa wakati mataifa yakiadhimisha siku ya lishe octoba 30 wilaya ya Rungwe itaadhimisha kwa kutoa elimu zaidi ya ulaji wa chakula kwa kuzingatia lishe bora kwa kundi la vijana balehe huku akitoa rai kwa wazazi kutenga muda wa kuhudumia familia zao.
Kuhusu ushiriki wa wanaume katika malezi yenye kuzingatia lishe bora afisa lishe amesema wazazi wengi wa kiume wanachukulia suala la lishe kuwa ni la mama pekee hivyo kuchangia katika kiwango cha udumavu kwa watoto wao.
Ikumbukwe kuwa maadhimisho ya siku ya lishe duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 30 octoba ya kila mwaka,na kwa mwaka huu 2023 kauli mbiu ni “lishe bora kwa vijana balee ni chachu ya mafanikio yao”.