Zaidi ya watoto laki moja kupata chanjo ya polio awamu ya pili Rungwe
24 October 2023, 2:44 pm
Baada ya kuvuka lengo kwa kuwafikia watoto zaidi ya elfu themanini chanjo ya polio awamu ya kwanza sasa wilaya ya Rungwe imejipanga kuwafikia zaidi ya watoto laki moja awamu ya pili
Na Sabina Martin – Rungwe
Zaidi ya watoto laki moja wenye umri chini ya miaka nane wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya polio awamu ya pili katika halmasahuri ya wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ili kuepuka ulemavu wa kudumu.
Akizungumza katika kipindi cha amka na chai kinachorushwa chai FM Dk. Mwajuma Ahmada kutokea wizara ya Afya amebainisha baadhi ya madhara yatokanayo na polio kuwa ni pamoja na ulemavu wa kudumu au kifo kwa watoto wasiochanjwa.
Pamoja na mambo mengine Dk. Mwajuma ametoa rai kwa wazazi na walezi kuwalinda watoto wao dhidi ya magonjwa yanayowashambulia watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa kuwapatia chanjo kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya.
Akizungumza kuhusu ugonjwa wa Polio Afisa program kutoka wizara ya Afya Bw. Penford Joel amesema hakuna tiba ya moja kwa moja kwaajili ya kutibu ugonjwa huo badala yake wataalamu wanashauri chanjo itumike zaidi.
Ezekiel Mvile ni mratibu wa chanjo wilaya ya Rungwe ameeleza kwamba zoezi la utoaji wa chanjo awamu ya kwanza ilikuwa ni kuwafikia watoto zaidi ya elfu themanini walifikia lengo na awamu hii ya pili wanatarajia kuwafikia watoto zaidi ya laki moja.
Kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka nane inatarajiwa kuanza rasmi tarehe 26 octoba hadi tarehe 29 octoba 2023, na kuwafikia watoto katika maeneo tofauti kama vile shuleni, kanisani, sokoni, nyumbani na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watoto.