Wazazi, walezi watakiwa kuwa karibu na wanafunzi wakati wa mitihani
13 September 2023, 1:16 pm
Wanafunzi wa darasa la saba wanatajia kufanya mitihani kote nchini hivyo jamii imeshauriwa kuwa sehemu ya watoto hao wakati wote ili wanafunzi waweze kufanya vizuri.
Na Bahati Obel – Rungwe, Mbeya
Wazazi na walezi wilayani Rungwe mkoani Mbeya wametakiwa kuhakikisha wanawasaidia watoto wanaofanya mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi kwa kuwaandalia mazingira rafiki yatakayowawezesha kufanya mitihani yao kama inavyohitajika.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rungwe Renatus Mchau amesema kuwa baada ya kuhitimu elimu ya msingi watoto wanatakiwa kuwa katika mazingira mazuri pamoja na kuwa na afya njema.
Aidha amewakumbusha wasimamizi wote wa mitihani katika halmashauri ya Rungwe kuhakikisha wanazingatia miongozo na sheria zilizowekwa ili kusiwe na hali inayoweza kutokea na kusababisha mitihani kutofanyika kama ilivyopangwa.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo halmashauri ya Rungwe ina jumla ya watahiniwa 7,296 wanaofanya mtihani wa taifa huku kukiwa na shule 145 ambapo kati ay hizo shule nne ni shule binafsi na shule 141 ni za serikali.
Taarifa iliyotolewa na katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) Dkt. Said Ally Mohamed imeeleza kuwa jumla ya watahiniwa 1,397,370 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kote nchini 2023.