Siku ya wanawake duniani itumike kufikia jamii zenye uhitaji
9 March 2022, 10:00 am
RUNGWE-MBEYA
NA:EZEKIEL KAPONELA
Siku ya Mwanamke duniani leo imeadhimishwa katika Halmshauri ya Wilaya ya Rungwe huku ikitolewa misaada mbalimbali kwa wahitaji.
Katika maadhimisho hayo yaliyokwenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu”mamia ya wanawake wamejitokeza huku wakitoa misaada kadhaa katika Gereza la Tukuyu na Shule ya msingi mchanganyiko Katumba II.
Wakiwa katika Gerera la Tukuyu wameshukuru uongozi wa gereza hilo kwa huduma wanayotoa kwani kwa kufanya hivyo wanasaidia kuijenga jamii kuishi katika maadili mema.
Akikabidhi zawadi hizo Afisa maendeleo ya Jamii wilaya ya Rungwe Bibi Inonsecia Miho amesema kuwa misaada hiyo itakuwa endelevu ikiwa ni sehemu ya kipato cha wanawake wanachozalisha kila siku na kukirejesha kwa jamii wakilenga kundi lenye mahitaji maalumu kama wafungwa, watoto yatima na walemavu.
Hata hivyo Mkuu wa Gereza la Tukuyu afande Anganile Mwakalobo ameshukuru kwa msaada huo uliotukuka na kuomba kuendelea kufanya hivyo kila mara kwani wafungwa katika gereza hilo wana mahitaji endelevu na gereza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali watasaidia kuzikwamua na hivyo kuongeza ustawi wa maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake Bupe Peter kutoka dawati la jinsia Wilayani Rungwe amesema bado dawati la jinsia linaendelea kutoa elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia sehemu mbalimbali.
Nao wanawake walioshiriki katika maadhimisho hayo wameshukuru Serikali kwakuendelea kuwaunga mkono wananwake na kuwapa nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya Vijiji,Kata,Wilaya,Mkoa hadi Taifa.