Chai FM

Chakula mashuleni chaongeza ufaulu Rungwe

8 November 2021, 6:22 am

RUNGWE-MBEYA

Ulaji wa chakula cha mchana katika shule za msingi wilayani Rungwe imechangia kuongeza kiwango cha ufaulu kwa matokeo ya darasa la saba mwaka huu kutoka asilimia 85.28 ya mwaka jana hadi asilimia 90.59 mwaka huu ambalo ni ongezeko la asilimia 5.31.

Akizungumza na Chai FM ofisini kwake afisa elimu msingi wilayani hapa Mwl. Gerald Kifyasi amesema kwamba ongezeko hili la ufaulu limechangiwa kwa kiasi kikubwa na  ushirikiano baina ya walimu pamoja na wazazi hususani suala la chakula shuleni.

Aidha amepongeza walimu wakuu katika shule zote wilayani Rungwe kwa namna walivyojitoa kuwafundisha wanafunzi kwa muda wa ziada na kuhakikisha wanapata chakula shuleni.

Katika hatua nyingine ametoa rai kwa jamii wilayani hapa kuanzia ngazi ya vijiji kuendelea kushirikiana ili wanafunzi wapate chakula shuleni kwani imeonekana kuongeza kiwango cha ufaulu katika mikoa mbalimbali kama vile Njombe na Iringa.