Pangani FM
Pangani FM
12/03/2026, 21:27

“Huku ni kuwarudisha nyuma wananchi na kuwavunja moyo waliacha kazi zao na kuchimba msingi wakiamini wanatengeneza kitu cha kuwasaidia lakini mpaka sasa malengo hayajatimia, lazima tuwasaidie wananchi kutatua changamoto zao, soko hili likikamilika wananchi wataongeza kipato chao na hayo ndiyo malengo ya chama cha mapinduzi.“
Na Cosmas Clement
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Tanga MCC Rajabu Abdulrahman ameamuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Pangani, ujenzi wa soko la Pangani Magharibi uliosimama kwa zaidi ya miaka kumi unakamilika haraka ili wananchi wapate sehemu nzuri ya kufanyia biashara.
Agizo hilo amelitoa March,12,2026 katika ziara yake alipotembelea miradi ya soko hilo pamoja na stendi ya daladala ya mji wa Pangani na kutoa kiasi cha shilingi milioni kumi kwa ajili ya kukamilisha mradi wa soko hilo.
MCC Rajabu ametaka soko hilo likamilike na kuanza kazi ifikapo mwezi wa tisa mwaka 2026 ili wananchi walitumie kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.

Ameagiza kuchukuliwe hatua madhubuti za kuzuia changamoto ya maji katika eneo hilo na kuanza kuhamasisha wafanyabiashara kuchukua maeneo ya kufanyia shughuli zao pamoja na kuweka utaratibu wa gulio.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya kijiji cha Pangani Magharibi inadaiwa kuwa Ujenzi wa soko hilo hapo awali ulianzishwa mnamo mwaka 2007 kupitia mradi wa TASAF na kutumika kiasi cha shilingi milioni 29 hata hivyo ujenzi wake ulisimama huku wananchi wakihusika katika kuchimba msingi wa soko hilo.