Pangani FM
Pangani FM
16 February 2026, 11:46 pm

“Hapo mwanzo tulikuwa tumepanga lakini baada ya migogoro yetu kuisha tumejenga nyumba na tumenunua shamba.“
Na Cosmas Clement
Uwezo wa wanandoa kushughulikia migogoro baina yao imetajwa kuwa chachu ya kuwawezesha kupiga hatua za maendeleo katika familia zao.
Hayo yamesemwa na wenza walioshiriki katika mafunzo saidizi yanayotolewa na shirika la UZIKWASA kwa wenza zaidi ya 28 kutoka maeneo mbalimbali wilayani Pangani.
Wakizungumza katika mafunzo hayo wenza hao wamesema kutokana na mabadiliko waliopata baada ya mafunzo ya wenza yamewawezesha kutatua migogoro iliyokuwa ikiwakabili hivyo kuwawezesha kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya familia.
Hata hivyo, wamesema mafunzo saidizi waliopatiwa hii leo yamesaidia kuwajengea uwezo wa kuondoa baadhi ya changamoto walizonazo ikiwemo kutokuaminiana.
Kwa upande wake Bwana Joseph Peniel mwezeshaji kutoka UZIKWASA amesema maelewano mazuri kwa wanandoa huwezesha kupanga kwa pamoja hivyo kupiga hatua katika maendeleo ya familia.