Wanafunzi watakiwa kuwa makini kipindi cha likizo ya Pasaka.
15 April 2022, 7:46 pm
Wito umetolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Pangani mkoani Tanga kuwa makini na kuzingatia tahadhari zote dhidi ya vishawishi vibaya katika kipindi hiki ambacho wapo kwenye mapumziko mafupi ya sikukuu za Pasaka.
Wito huo umetolewa na afisa elimu taaluma kwa shule za sekondari Wilayani Pangani mwl. MUSSA LIKU wakati akizungumza na kituo hiki.
Katika kipindi cha likizo kumekuwa na changamoto ya wanafunzi kujikuta katika masuala hatarishi kama kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo yanayopelekea kupata ujauzito, ubakaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha mwalimu Mussa ametoa wito pia kwa wazazi kuwalinda watoto wao ili kuhakikisha wanakuwa salama dhidi ya vitendo vya ukatili na kuwahamasisha kuendelea kulinda ndoto zao hususan zinazotokana na mafanikio ya kitaaluma.
.
Pia amewashauri wazazi ambao watoto wao wanasoma shule za bweni kuona umuhimu wa kuwapima afya ya mwili na akili ili kujua hali ya afya zao.