Waliojitokeza kupokea chanjo ya Corona Pangani.
4 August 2021, 5:37 pm
Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga leo imeanza zoezi la utoaji wa Chanjo ya virusi vya Corona kwa makundi yaliyopewa kipaumbele ikiwemo watoa huduma za afya, watu wenye magonjwa sugu na wazee.
Viongozi wa Serikali, taasisi, watumishi wa afya na wananchi mbalimbali wamejitokeza katika zoezi hilo la uzinduzi wa utoaji chanjo za Virusi vya Corona kwa Wilaya ya Pangani.
Zoezi hilo limefanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani leo Jumatano Agosti 4 mwaka 2021.
Akizungumza na Pangani FM Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Dokta Maulid Majala amesema wamepokea Dozi 1000 za Chanjo ya Corona na amewasisitza Wananchi kujitokeza kupata chanjo hiyo kwani ni salama.
Ndani ya muda usiozidi saa 2, kuanzia saa 7 mpaka saa 9 mchana leo idadi ya watu 59 wamepokea chanjo hiyo kwa Wilaya ya Pangani.
Mwanahabari wetu Maajab Madiwa amefika katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani na kuzungumza na Viongozi mbalimbali waliojitokeza katika tukio hilo.
Sikiliza hapa taarifa hii.
Siku chache zilizopita Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi kampeni ya taifa ya chanjo ya Covid-19 na kuwa wa kwanza kuchanjwa ambapo aliwahakikishia Wananchi kuwa Chanjo hiyo ni salama, wakati mjadala kuhusu chanjo ukihanikiza.
Tayari viongozi katika maeneo mbalimbali nchini wameanza kupokea chanjo hizo.