RC Tanga: Hakikisheni mpaka June 28 hoja 19 zimejibiwa
22 June 2024, 10:37 am
Pamoja na kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 halmashauri ya wilaya ya Pangani imekuwa na hoja nyingi ambazo hazijajibiwa ikiwemo kumi na tisa za kamati ya kudumu ya Bunge.
Na Cosmas Clement
Halmashauri ya wilaya ya Pangani imepewa siku sita kuanzia Jumamosi ya leo kujibu hoja kumi na tisa za kamati ya kudumu ya Bunge zilizotolewa katika ripoti ya mkaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Batilda Buriani katika kikao cha Baraza la madiwani cha kujadili na kupitia hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali katika kipindi cha mwaka fedha uliopita.
Awali akiwasilisha taarifa ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali, Bwana Gudlucky Minja amesema halmashauri ya Wilaya ya Pangani ina hoja zipatazo thelathini na tisa ambazo hazijajibiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Pangani Bwana Edward Charles Fussi amesema halmashauri imepokea maelekezo hayo na inaendelea kufanyia kazi kujibu hoja hizo.
Pamoja na hoja hizo kutojibiwa, halmashauri ya wilaya ya Pangani katika kipindi cha mwaka fedha 2022/23 imefanikiwa kupata hati safi ambayo inakuwa ni mwaka sita mfululizo kupata hati hiyo.