DC Kilakala: Mzee anayetongoza wavulana akamatwe
17 June 2024, 9:20 am
Matukio ya ulawiti kwa watoto wa kiume yamekuwa yakitajwa kuongezeka na yakitajwa kutekelezwa na watu wakubwa, huku vijana wakijifunza kutoka kwa wakubwa.
Na Hamisi Makungu
Vyombo vya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga vimeagizwa kumkamata Mzee mmoja anayetuhumiwa kuwashawishi watoto wa kiume kwa lengo la kuwafanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani MUSA KILAKALA ambaye ndiye Mgeni rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Kiwilaya ambayo yamefanyika tarehe 16 juna 2024 katika Shule ya Sekondari Bushiri.
KILAKALA amesema Serikali haiwezi kulikalia kimnywa suala hilo, huku akitaka mzee huyo kuhojiwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Agizo hilo la Mkuu wa Wilaya limejiri kufuatia Mtoto mmoja ambaye amenusurika kufanyiwa ukatili na Mzee huyo kutoa maelezo hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya.
Awali akisoma Risala kwa niaba ya watoto wa Pangani mbele ya Mgeni rasmi kwenye Maadhimisho hayo Fatuma Abdi Mwanafunzi wa Kidato cha Pili Shule ya Sekondari Bushiri ameomba wazazi, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuungana kwa pamoja katika kumlinda mtoto dhidi ya changamoto za ukatili wa kijinsia.
Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo wa Wilaya Bi. Nsekela Steven Mwalukasa amesema katika kipindi cha kuanzia Mwezi JuneMwaka jana hadi Mei Mwaka huu jumla ya kesi 33 za ukatili wa kijinsia zimeripotiwa Polisi, huku watuhumiwa wawili wa kesi za ukabaji wakihukumiwa kifungo cha Miaka 30 jela kila mmoja.